Buriani Ruge Mutahaba


Ruge Mutahaba amefariki Afrika kusini alikokuwa akipokea matibabu

Serikali nchini Tanzania kupitia Rais wake John Pombe Magufuli imekiri kupokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Ruge Mutahaba aliyekua mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group Tanzania.

Ruge alikua moja kati ya watu wenye mchango mkubwa katika tasnia ya habari burudani, na ni mtu aliyekua mwenye juhudi za kujenga fikra za maendeleo ya vijana Tanzania.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter, Rais Magufuli aliandika taarifa yake huku akitoa pole kwa familia , ndugu jamaa na marafiki zake wa karibu wakiwemo wasanii nchini Tanzania.


Ruge Mutahaba alikua Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group Tanzania ambao ni washirika wa baadhi ya vipindi vya BBC amefariki dunia usiku wa Februari, 26 akipatiwa matibabu nchini Afrika Kusini.

Muasisi mwenza na Mkurugenzi mtendaji wa Clouds Media Group Joseph Kusaga ameeleza namna ambavyo Ruge atakumbukwa na anachokiacha nyuma.

'Ruge ametutoka akiwa bado kijana mdogo kabisa, amefanya mambo mengi sana. Amepigana ameugua, amekuwa South Africa kwa muda tukipigania sana kuhakikisha anarudi katika hali yake ya kawaida, afya bora.

'Lakini Mungu amempenda na amemchukua siku ya leo, amueke mahali pema peponi'.

Mutahaba alizaliwa Mwaka 1970 huko Brooklyn nchini Marekani

Akapata elimu ya msingi huko Jijini Arusha Kaskazini Mwa Tanzania baadae akajiunga na Shule ya Sekondari ya forodhani katika mji wa Dar es salaam pamoja na Pugu.

Lakini hapo baadae alirejea tena Nchini Marekani kwa masomo ya elimu ya juu zaidi ikiwemo shahada ya uzamili na uzamifu.

Hakuna maoni

Inaendeshwa na Blogger.